Saturday, February 8, 2020

JOKA LA MDIM
UCHAMBUZI WA KAZI  YA FASIHI SIMULIZI
JOKA LA MDIM
KIPENGELE CHA FANI.
ZINGATIA:
1. (katika uchambuzi huu mwanafunzi atatakiwa kufahamu muundo na mtindo wa kitabu pamoja na matumizi ya lugha ili kujibu maswali yatayohusiana na kipengele hiki)
2. (matumiz,  ya lugha hujumuisha lugha za picha, misemo,nahau na tamathali za semi katika kuwakilisha kazi zao)
3. (kumbuka katika uchambuzi wa vitabu hutumika wakati uliopo(simple present) na hii ni pale unaponukuu baadhi ya maneno katika kitabu)
4.( kuna namna ya kuandika utangulizi(introduction) wakati wa kujibu swali lolote linalohusiana na kitabu cha kuzingatia ni kwamba swali linataka nini ) kwa mfano angalia swali hili "waandishi wengi wa vitabu wamekuwa wakiyaona mambo katika jamii na kuyakosoa ili jamii ibadilike, tumia riwaya mbili ulizosoma kudhihirisha hili"
1. je umefahamu swali linataka nini ? (ujumbe?, maudhui?,au migogoro?)
2.je ni kwa vipi ungeonyesha riwaya utazotumia ?
3. je utaanza na riwaya gani, na utamaliza na ipi ?
4.je utahitimisha vipi insha yako ?
5. je utatumia mifano(quotation) unapotetea hoja zako?
MWANDISHI: ABDALLAH J. SAFARI
MCHAPISHAJI : HUDA PUBLISHERS
MWAKA: 2007
JOKA LA MDIMU image
UTANGULIZI WA KITABU
Joka la mdimu ni riwaya iliyojengwa kwa visa tofautitofauti vinavojengana kukamilisha masimulizi. Ni riwaya inayosawiri au kuakisi mambo yaliyopita ya nyakati za nyuma ambapo kulikuwa na shida kama vile za mafuta ya petroli, Nguo, vyakula nk. Pamoja na hayo zipo pia dhamira au mawazo ambayo yanasawiri maisha ya Mtanzania wa leo kama vile masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Kwa upande wa fani ni riwaya ambayo mwandishi amewaumba vyema wahusika wake kwa kuwavika uhalisia vyema, amepanga visa vyake na amejitahidi kutumia lugha yenye mvuto na vionjo vya kisanaa huku akiwaburudisha wasomaji  kwa mtindo wa kipekee.
JINA LAKITABU
Jina la kitabu limewekwa katika lugha ya picha, JOKA LA MDIMU ni nyoka anayeishi katika miti ya kijani. Nyoka huyu hupendelea kuishi katika miti ya Minyaa na Midimu inayofanana na rangi yake. Nyoka huyu awapo kwenye miti hiyo si rahisi kumtambua kutokana na rangi yake kufanana sana na miti hiyo. Hivyo ni nyoka hatari sana kwa binadamu.
Mwandishi anatumia taswira ya Joka la Mdimu kufananisha na viongozi ambao ni wananchi wenzetu, wanafanana na sisi, ni ndugu zetu damu yetu. Lakini ni hatari mno kwani hutugeuka na kuwa mafisadi, wala rushwa, hawatimizi majukumu yao, ni walaghai nk. Badala ya kusaidia wananchi wao hujali maslahi yao kwanza na hivyo kusababisha mifumo ya kiuchumi kuendelea kuwa migumu kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha watu walio maskini au hohehahe. Hivyo jina la kitabu linasawiri yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii.
FANI
MUUNDO
Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo changamani yaani kwa kiasi fulani ametumia rejea au rukia pia ametumia muundo sahili au msago.
Mfano ametumia muundo wa rejea katika sura ya Mindule ambapo anaanza kutueleza juu ya habari za Amani dereva wa taxi na adha anazopata kutokana na ukosefu wa mafuta na jinsi anavyoiendesha biashara yake hiyo. Lakini ndani ya sura hiyohiyo anaturudisha nyuma na kuanza kutuelezea namna Amani alivyopata kazi ya udereva Taxi na kutueleza juu ya mmiliki wa Taxi hiyo ambaye ni Shiraz Bhanj. Pia katika sura ya Boko anatueleza juu ya Safari ya Tino kwenda kumuona mwanae mgonjwa uk.73 ila hatuelezi inavyoendelea lakini anarukia kisa kingine cha Brown Kwacha na sura ya Kwale halafu badae anaturudisha nyuma na kuendelea kutuelezea juu ya habari za kuuguliwa kwa Cheche na Tino anapofika kumuona katika sura ya Dakta Makwati. Pia ametumia muundo wa moja kwa moja katika sura zingine kwani ameyapanga matukio yake katika usahili bila kuruka.
Pia mwandishi amegawanya visa na mtukio katika sura kumi ambapo kila sura ameipa jina kwa kutumia majina ya wahusika.
Sura ya kwanza, MINDULE
Hapa mwandishi anatueleza kuhusu habari za Amani dereva Taxi, masaibu anayopata katika kazi yake kutokana na uhaba wa mafuta katika vituo vya mafuta.
Sura ya pili, TINO
Hapa tunaelezwa kuhusu maisha ya Tino na kazi anazofanya ya kuvuta kwama. Tunaambiwa kuhusu hali ngumu ya maisha ya Tino na wakazi wengine wa Sega, hapa tunaelezwa pia kuhusu masuala ya uongozi jinsi ulivyo mbovu na ugawanywaji mbovu wa vyanzo vya uchumi na bidhaa.
Sura ya tatu, JINJA MALONI
Katika sura hii tunaelezwa kuhusu maisha ya Jinja Maloni, hapa anaibua dhamira kama vile za uvamizi, uhalifu na mauaji pia anaendela kutueleza kuhusu hali ngumu ya maisha.
Sura ya nne SEGA
Maisha ya wakazi wa Sega yanaelezewa hapa jinsi yalivyo ya dhiki, pia tunaelezwa kuhusu Tino na mkewe maisha yao yalivyo na familia yao, anaibua dhamira ya mapenzi ya dhati na upendo kwa familia.
Sura ya tano, BOKO
Hapa tunaelezwa kuhusu adha ya usafiri kwa watu, shida ya mafuta, ubovu wa miuondmbinu kama vile barabara, vinasemwa hapa.
Sura ya sita, BROWN KWACHA
Sura hii inaeleza habari za Brown maisha yake na tabia zake, anaibua dhamira kama vile uhujumu uchumi, biashara za magendo, suala la kutowajibika kwa watumishi, suala la kukosekana kwa uaminifu katika ndoa na mapenzi ya pesa ambapo sifa zote hizi alizibeba Kwacha.
Sura ya saba, KWALE
Hapa yanaelezwa mambo kuhusu hifadhi ya Kwale, safari ya Brown na Leila kwenda kutembea kwale. Hapa yanatajwa mambo ya udhalimu wa kuharibu mali za umma (maliasili za taifa) mfano pembe za ndovu, vipusa pia mapenzi yasiyo ya kweli.
Sura ya nane, DAKTA MIKWALA
Dakta Mikwala ndiye mhusika mkuu anayeelezwa hapa, tunalezwa juu ya ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya kwani Cheche anashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.
Sura ya tisa, CHECHE
Tunaelezwa juu ya juhudi za Amani na Tino ili kumsaidia Cheche aweze kwenda kutibiwa Uingereza. Wanafanikiwa kupora benki na kupata pesa za kumtibu Cheche.
Sura ya kumi, MOTO
Hapa hatma ya visa vidogo vidogo imeelezwa kwa kutolewa hatma ya maisha ya Cheche na Brown Kwacha. Cheche alipata matibabu na kupona na Browna anafanikiwa kuirubuni serikali kwa kuipanga mahesabu ya uongo.
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo ya aina tofautitofauti ili kuweza kuipamba kazi yake ivutie.
Matumizi ya nafsi.
Matumizi ya nafsi ya tatu Umoja. Imetawala.
Mfano uk.5 Amani aliangalia. Uk.25 Amani alijizuia .
Nafsi ya tatuwingi; mfano uk. 63  wote walitoka nje kuelekea klabuni.
Pia uk.53 wale wanaume walimvamia
Matumizi ya nafsi ya pili.
Mfano uk.106  mmechoka kuangalia video? aa tumeshaziona mara nyingi tunaomba aina nyingine . Mazungumzo baina ya mke wa Brown na wanae.
Pia mazungumzo baina ya Brown na Leila.
Uk.113. habari za asubuhi
 Nzuri sijui wewe alijibu
Uliota njozi njema?
"Wapi?"
"Kwa nini?"
Matumizi ya nafsi ya kwanza.
Mfano uk. 39 mimi nimemaliza .kuiba nimeiba sana.
Matumizi ya nyimbo. Uk . 70 . wimbo wa Chaupele
Chaupele mpenzi, haya usemayo
Kama ni maradhi, yapeleke kwa Daktari
Wanambia niache rumba, na mimi sikuzoea
Sitaweza kuliacha rumba, kwa sababu yako
Kama wanipenda, nenda kwa baba
Pia uk.58 sega! Sega! Sega!, usioogope  wimbo waliouimba washabiki wa michezo.
Masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi.
Hapa mwandishi amemtumia muhusika kusimulia kisa kingine kidogo ndani ya kisa kikuu. Mfano uk . 39 mhusika Tino anamsimulia mteja wake maisha yake ya mwanzo kabla hajaanza kazi ya kuvuta kwama.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi A. Safari ametumia lugha fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji wake. Kuna matumizi ya lugha nyinginezo kama vile kiingereza. Uk.55 city devils uk.155 I miss my family, uk.24 Hey man you will pay extra money, uk.99 consignment. Pia kuna matumizi ya lugha ya kiarabu, mfano uk.45 Salaam aleikum mayitun uk.42 Inna Ilayhi Raajiunna!, uk.13, Insha Allah! . Vilevile kuna matumizi ya lugha ya mtaani uk.39 msela, ndito, kashkash.
Matumizi ya tamathali za semi.
Tashibiha
Uk.117 ngozi yake nyeusi kama udongo wa mfinyanzi
Uk.122 mweusi kama sizi la chungu
Uk.9 Zepher 6 ile iliunguruma kama simba dume
Uk.10 mteuzi mithili ya Mbega
Uk.35 miguu yake ikakazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa
Sitiari
Uk.91 Brown Kwacha alikuwa kinyonga
Uk.15 sarahange wetu mboga kweli siku hizi
Uk.40 huku twakaa vinyama vya mwitu
Uk.72 sote ni kobe
Tashihisi
Uk.109 gari lile zuri lilioondoka kwa madaha
Uk.143  kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama twe!kuomboleza
Uk.91 pua zake zikalakiwa na riha na ashrafu ya manukato
Uk.12 utumbo ulimlaumu
Uk.27 mvua ikapiga kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu.
Tafsida
Uk. 49 isijekuwa nimekukatiza haja!, pia uk. hohuo kinyesi.
Mbinu nyingine za kisanaa.
Takriri
Uk.151 mwizi! Mwizi! Jambazi! Jambazi!
Uk.57 shinda! Shinda! Shinda!
Uk.33 karibu baba, kariibu kaka, karibu mkwe
         Uk.72 uhuru upi? Uhuru gani? Uhuru wa nini na nani?
Mdokezo
Uk.149 lakini..
Onomatopea au tanakali sauti
Uk. 1 saa mezani niliendelea kugonga taratibu ta! ta! ta!
Uk.10 ikatoka sauti kali tupu ta nye nye
Uk.67 upepo wa stova uliolia shshsh
Tashtiti
Uk.113 . leila anamuuliza Brown maswali ambayo anayajua majibu yake.
Brown: uliota njozi njema?
Leila : Wapi?
Leila: Kwanini?
Brown: Mwenywe unajua
Nidaa
Uk.39 Aaa! Limbukeni wa jiji anataka kunitia kashkash
     Uk 30 nguo zangu Mungu wee!
Uk.42 Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiunna!
Uk.92 Ah! Leila kwacha alimsalimia kwa furaha
Uk. 105 Lahaula
Matumizi ya Semi.
Methali
Uk.78 asilojua mtu ni usiku wa kiza
Uk.83 ukiona mwenzako anyolewa zako tia maji
Uk.98 mtaka waridi sharti avumilie miiba
Uk. 99 biashara haigombi
Uk.43 ajizi nuksani huzaa mwana kisirani
Misemo
Uk.10 asiye na bahati habahatishi
Uk.47. asiyezika hazikwi
Uk.64 mmetupa Jongoo na mtiwe
Uk.98 asali haichomvwi umoja
Uk.111 ajali haina kinga
Uk.115 mwenye macho haambiwi tazama
Uk.120 matendo hushinda maneno
Uk.47. asiyezika hazikwi
Nahau
Uk.11 sio unanilalia kila mara  kunidhulumu
Uk.107 alikonda akajipa moyo  kujifariji moyo
Matumizi ya taswira
Taswira mwonekano imetumika, ambayo inatujengea picha kutokana na vitu tunavyovifahamu. Mfanouk.76 alisema kijana mmoja wa kiume kavaa sketi, blauzi na sidiria iliyopachikwa juu yake. Kichwani alifunga kilemba. Hii inatupa picha halisi ya huyo kaka kwani tunaposoma ni kama kweli tunamuona kutokana na jinsi mwandishi alivyoelezea. Pia uk.135 mwambie yule jamaa pale atayarishe kuku mzuri wa kukaanga na kachumbari yenye pilipili hii inamfanya msomaji ahisi ladha ya kuku na hiyo pilipili kwa maneno ambayo mwandishi ameyajengea taswira na hii ni taswira hisi.
la mdimu ni taswira ya nyoka mbaya ambaye amefananishwa na viongozi wabaya.
WAHUSIKA
AMANI
Ni dereva taxi
Ana upendo wa dhati
Ni mchapakazi
Ana hekima na busara
Ana huruma
Ni rafiki wa kweli wa Tino
Kutokana na hizo sifa amani ni mhusika bapa
Anafaa kuigwa na jamii
TINO ( mhusika bapa )
Ni mchapakzi
Mlezi bora wa familia
Baba wa Cheche
Ana huruma
Ana upendo wa dhati
Ni makini
Ni jasiri
Ni mwanamichezo
Anafaa kuigwa na jamii
BROWN KWACHA
Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni
Ni muhuni na Malaya
Fisadi na mla rushwa
Anafanya biashara haramu
Hana mapenzi kwa familia yake
Anapenda anasa
Si muaminifu kwa mkewe
Si muadilifu
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa
JINJA MALONI
Ni jasiri na mwenye nguvu
Ana huruma na upendo
Mchapakzi
Mlevi
Maskini
Ni mhusika duara
DAKTARI MIKWALA
Ni daktari bingwa wa mifupa
Anapenda rushwa
Si muwajibikaji katika kazi yake
Ni mlevi
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa
SHIRAZ BHANJ
Ni mfanyabiashara
Ni mtoa rushwa
Ana biashara za magendo
Rafiki wa Brown
Hafai kuigwa na jamii
Ni mhusika bapa
ZITTO
Ni mfanyakazi bandarini
Ni mwanamichezo
Ni jasiri ana kipato duni
Rafiki wa Tino na Amani
CHECHE
Ni mtoto wa Tino
Ana nidhamu na bidii
Ni mwanamichezo
Ana upendo kwa wazazi wake
Ni mtiifu na msikivu
Mcheshi na mudadisi
Alivunjika kiuno michezoni
Ni mhusika bapa
MWEMA
Ni mke wa Tino
Mvumilivu
Ana mapendo ya dhati kwa familia yake
Ni mchapakazi
Ni mhusika bapa
JOSEPHINE NA LEILA
Wasichana wahuni waliojiuza kwa Brown Kwacha
Hawafai kuigwa na jamii
MANDHARI
Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, anataja baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kama vile Boko, Sega, Mindule. Mandhari hii ni sadifu kwa yale ambayo mwandishi ameyaeleza kwani masuala ya rushwa, upotevu wa haki, hali ngumu ya uchumi na maisha kwa ujumla, ni matatizo halisi ya jamii ya Tanzania

No comments:

Post a Comment